Skip to main content

Sehemu Ya Bajeti Ya Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Usafiri Na Uchukuzi Kwa Njia Ya Anga) - 2017/2018

Ifuatayo ni sehemu ya bajeti ya wizara ya uchukuzi kwa upande wa usafiri na uchukuzi kwa njia ya anga kwa mwaka 2017/2018 kama ilivyowasilishwa na waziri Profesa Makame Mbarawa katika bunge la bajeti mjini Dodoma.USAFIRI NA UCHUKUZI KWA NJIA YA ANGA

Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga

154.Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuzingatia vigezo na kanuni za usalama wa usafiri wa anga kama inavyoshauriwa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (The International Civil Aviation Organisation-ICAO). Kwa lengo la kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini. Wizara kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imeendelea kusajili ndege kulingana na masharti ya usajili ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi, 2017, ndege 14 zilisajiliwa kwa mara ya kwanza hapa nchini na ndege 79 zilikaguliwa na kupewa vyeti vya ubora wa kuendelea kufanya kazi. Lengo ni kuhakikisha utekelezaji wa sheria na kanuni za Usalama wa Usafiri wa Anga zinafuatwa.

155.Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TCAA imeendelea kudhibiti ajali za vyombo vya usafiri wa anga. Katika mwaka 2016/2017, hakuna ajali ya usafiri wa anga iliyotokea isipokuwa yalikuwepo matukio saba (7) ya vyombo vya usafiri wa anga. Aidha, Mamlaka imeendelea kuimarisha usalama katika viwanja vyote vya ndege ili kuhakikisha kwamba viwanja hivyo havitumiki katika matukio ya uhalifu yakiwemo ya kupitisha madawa ya kulevya na nyara za Umma. Pia, Mamlaka imeendelea kuhakikisha kwamba maafisa wa usalama katika viwanja vya ndege wanapatiwa mafunzo stahiki na kupewa leseni. Katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017, jumla ya maafisa usalama 35 walipatiwa mafunzo. Kati yao, maafisa 25 walihitimu na kupewa leseni.

156.Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Mamlaka ya Usafiri wa Anga iliendelea kufanya kaguzi za viwanja vyote vya ndege nchini ili kuhakikisha kuwa viwanja hivi vinakidhi vigezo, masharti na kanuni zilizowekwa na Mamlaka. Viwanja vya ndege vilivyokaguliwa na kupewa vyeti vya ubora baada ya kukidhi vigezo vya kimataifa kwa ajili ya kupokea ndege kubwa ni pamoja na Julius Nyerere, Amani Abedi Karume na Kilimanjaro. Aidha, uimarishaji na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Pemba, Geita, Matemanga na Jengo la Tatu la Abiria katika kiwanja cha Julius Nyerere uliendelea kudhibitiwa ili kukidhi viwango vya usalama.

157.Mheshimiwa Spika, Ili kudhibiti na kuimarisha usalama wa usafiri wa anga nchini, TCAA inatarajia kununua rada 4 za kuongozea ndege za kiraia. Majadiliano ya mkataba baina ya TCAA na Mkandarasi (M/s Thares Air Systems) kutoka Ufaransa yanakamilishwa na mkataba unatarajiwa kusainiwa wakati wowote. Rada hizi ambazo zitakamilika usimikaji wake Aprili, 2018 zitafungwa katika viwanja vya ndege vya JNIA, Mwanza, Kilimanjaro na Songwe kwa gharama ya Shilingi bilioni 61.3.

158.Mheshimiwa Spika, utendaji wa sekta ya usafiri wa anga nchini umeendelea kukua. Katika mwaka 2016/2017, idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga imefikia abiria 5,057,180 ikilinganishwa na abiria 4,861,277 waliosafiri mwaka 2015/2016. Hili ni ongezeko la asilimia 4. Kwa abiria wanaosafiri kwenda na kutoka nje ya nchi, katika mwaka 2016/2017, jumla ya abiria 2,238,653 wanatarajiwa kusafiri ikilinganishwa na abiria 2,146,360 waliosafiri katika mwaka 2015/2016. Sababu za ongezeko hili ni pamoja na kusainiwa kwa mikataba ya usafiri wa anga kati ya Tanzania na nchi zingine (Bilateral Air Services Agreements - BASA); uimarishaji wa miundombinu na huduma za viwanja vya ndege; uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA); ukuaji wa uchumi na shughuli za utalii nchini. Aidha, idadi ya abiria waliosafiri ndani ya nchi imeongezeka kutoka abiria 2,910,820 mwaka 2015/2016 hadi abiria 3,056,361 katika mwaka 2016/2017. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 5. Sababu ya ongezeko la abiria wa ndani ni pamoja Serikali kutekeleza azma yake ya kuimarisha na kuendeleza Kampuni ya Ndege Tanzania, kukua kwa shughuli za kiuchumi, kuongezeka kwa utalii nchini na kuanzishwa kwa safari za ndege katika maeneo mapya ya Dodoma, Bukoba na Songea.

159.Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma za kusafirisha mizigo katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini umeendelea kukua. Hadi Aprili, 2017, mizigo ya kwenda na kutoka nchini ilifikia tani 32,773.6 kutoka tani 31,425.2 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2015/2016. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 4.3. Ongezeko hili lilichangiwa na kukua kwa shughuli za kibiashara na kiuchumi ndani na nje ya nchi na jitihada za kuboresha miundombinu ya huduma za usafirishaji wa mizigo kupitia usafiri wa anga.

160.Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017, jumla ya kampuni 59 zilipewa leseni kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali katika viwanja vya ndege. Kati ya hizo, Kampuni 25 zilipewa leseni ya kutoa huduma mbalimbali kwa kampuni nyingine za ndege (Third Party Ground Handling Services Providers); Kampuni 14 kutoa huduma kwenye ndege zake zenyewe (self handling); Kampuni 8 kutoa huduma za vyakula kwa kampuni za ndege na Kampuni 12 kutoa huduma ya ugavi wa mafuta ya ndege. Aidha, hadi Machi, 2017, jumla ya kampuni za usafiri wa ndege 61 zilikuwa zinatoa huduma za usafiri wa anga wa ratiba (scheduled) na usiokuwa wa ratiba (non-scheduled air services). Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 5 ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka 2015/2016.

161.Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuingia makubaliano ya huduma za usafiri wa anga na nchi mbalimbali (BASA) kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko na kurahisisha usafiri katika sekta hii muhimu. Katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Aprili, 2017, jumla ya makubaliano mapya kumi (10) yaliingiwa baina ya Tanzania na nchi za Israel, Ureno, Guyana, Canada, Norway, Sweden, Morocco, Falme za nchi za Kiarabu, Denmark na Uganda. Aidha, mikataba ya nchi nne (4) za Malawi, Kenya, Oman na Uturuki ilipitiwa upya. Makubaliano haya yanafanya hadi Aprili, 2017, Tanzania kuwa imeingia mikataba ya BASA na jumla ya nchi 68 ikilinganishwa na nchi 60 zilizokuwa zimesaini makubaliano hayo mwaka 2015/2016. Hadi Aprili, 2017, Mashirika ya ndege ya kimataifa ya ndani na nje ya nchi 29 yalikuwa yanatoa huduma za usafiri wa anga kwa utaratibu wa BASA. Aidha, safari za ndege kati ya nchi hizo na Tanzania zilikuwa 193 kwa juma.

162.Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa gharama za mawasiliano ya ndege kati ya kituo na kituo zinapungua na zinakuwa za uhakika. Moja ya uboreshaji huo ni kubadilisha mfumo wa mawasiliano ya anga kutoka mfumo unaotumika sasa wa analojia kwenda mfumo wa digitali. Kazi ya kuboresha mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani wakiwa angani (VHF area cover relay station) huko Lokisale, Arusha na Changarawe, Iringa zimekamilika. Aidha, zabuni ya kuboresha mfumo wa mawasiliano kwenda mfumo wa digitali wa ufuatiliaji wa safari za ndege katika kituo cha Pemba ilitangazwa Februari, 2017.
Kuhusu kufanya ukarabati wa mnara wa kuongozea ndege katika kituo cha Pemba, zabuni ya kumpata mkandarasi wa kufanya ukarabati wa mnara huo zilifunguliwa tarehe 2 Februari, 2017. Kazi za ukarabati zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika Juni, 2017.

163. Mheshimiwa Spika, kuhusu mfuko wa mafunzo kwa marubani na wahandisi wa ndege, Mamlaka ya TCAA inaendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kuweza kufadhili wanafunzi wengi zaidi kwenye mafunzo ya urubani na wahandisi wa ndege. Hata hivyo, Mamlaka inaendelea kushirikiana na vyuo vingine hapa nchini kikiwemo Chuo cha Usafirishaji (NIT) ili kuhakikisha kwamba mafunzo hayo yanatolewa hapa nchini.

Huduma za Viwanja vya Ndege
164.Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) imeendelea kuboresha miundombinu na huduma za viwanja vya ndege nchini ili kuwezesha ndege kubwa na ndogo kutua na kuruka kwa usalama. Uboreshaji huo unalenga kuviwezesha viwanja vya ndege nchini kutumika kwa majira yote ya mwaka na kuvutia mashirika mengi zaidi ya ndege nchini ili kuongeza ushindani na hivyo kupunguza gharama za usafiri wa Anga.
165.Mheshimiwa Spika, ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika Desemba 2017. Jengo hilo limeezekwa na kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kuta za ndani ya jengo, usimikaji wa madaraja ya abiria kupandia/kushukia kwenye ndege, mifumo ya viyoyozi, miundombinu ya umeme, mifumo ya maji safi na maji taka pamoja na mifumo ya zimamoto. Aidha, ujenzi wa maegesho ya ndege umefikia hatua ya matabaka ya lami. Kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza uwezo wa kiwanja kuhudumia hadi abiria milioni 8.5 kwa mwaka kutoka abiria milioni 2.5.

166.Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia uendeshaji na uboreshaji wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro ili kuhakikisha kinakuwa bora na kuchangia katika ukuaji wa biashara za maua, mbogamboga, matunda na utalii. Kazi za ukarabati wa kiwanja hiki zimekamilika kwa asilimia 70 na ujenzi unatarajiwa kukamilika Mei, 2017. Aidha, magari mawili mapya, makubwa na ya kisasa ya zimamoto yalinunuliwa. Kukamilika kwa ukarabati wa KIA kutaongeza uwezo wa barabara ya kuruka na kutua ndege kuhudumia ndege nyingi na jengo la abiria kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka kutoka abiria 500,000 wa sasa.

167.Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza uliendelea kutekelezwa. Hadi kufikia Machi, 2017 hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa kazi za kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege kwa mita 500. Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa jengo la kuongozea ndege, ujenzi wa jengo la mizigo na maegesho ya ndege.

168. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TAA inaendelea na awamu ya pili ya ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora. Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya pili ya kutua na kuruka ndege (secondary runway), eneo la maegesho ya ndege (apron), barabara ya maungio (taxiway) kwa kiwango cha lami, usimikaji wa mitambo ya kuongozea ndege (NavAids, DME na VOR) na taa za barabara ya kurukia ndege (AGL). Kazi za ukarabati wa Kiwanja hiki zilianza Septemba, 2016 na zinatarajiwa kukamilika Juni, 2017.

169. Mheshimiwa Spika, kuhusu ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Kigoma, Benki ya EIB ilitoa kibali (No Objetion) cha kutangaza upya zabuni ya ukarabati Machi, 2017 kufuatia gharama za wazabuni kutokuwa shindani. Zabuni ya marejeo inatarajiwa kutangazwa Mei, 2017. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Jengo la Abiria pamoja na miundombinu yake (maegesho ya ndege, maegesho ya magari na barabara ya kuingia na kutoka), usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege, ujenzi wa uzio wa usalama na jengo la uchunguzi wa hali ya hewa (OBS).

170. Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba na kuanza kutumika, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imekamilisha ujenzi wa shule mpya ya msingi katika eneo la Mafumbo. Madhumuni ya ujenzi wa Shule hii ni kuweka mazingira mazuri ya utoaji wa huduma za usafiri wa anga bila kuathiri utoaji elimu. Ujenzi wa shule hii ulikamilika Aprili, 2017.

171. Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizoendelea kutekelezwa katika mwaka 2016/17 ni pamoja na:
i.Usimikaji wa taa za kuongozea ndege wakati wa kutua (PAPI) katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe ulikamilika Novemba, 2016;
ii.Kazi ya kumpata Mkandarasi kwa ajili ya kuanza kazi za ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga zilikamilika Machi, 2017. Ukarabati wa viwanja hivyo utaanza Mei, 2017;
iii.Nyaraka za manunuzi ya Mtaalam Mwelekezi wa kazi ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa miundombinu ya Kiwanja kipya cha Ndege cha Msalato zimewasilishwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kupata “No Objection”. Kazi hii inatarajiwa kuanza Agosti 2017;
iv.Kazi za upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege kumi na moja (11) vya Lake Manyara, Musoma, Iringa, Tanga, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Simiyu na Singida kwa kiwango cha lami. Kazi hizo zitakamilika Mei, 2017;
v.Kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Jengo la pili la abiria (TBII) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere imekamilika. Serikali inaendelea na majadiliano na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kupata fedha za utekelezaji wa mradi huo.

Huduma za Usafiri wa Anga
172.Mheshimiwa Spika, huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi zimeendelea kutolewa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) pamoja na Kampuni za sekta binafsi zikiwemo Precision Air, Fastjet, Auric na Coastal Air.

173.Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza azma yake ya kufufua na kuboresha huduma za Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) ili kusaidia kukuza sekta nyingine za kiuchumi ikiwa ni pamoja na utalii, biashara, madini na kilimo. Katika mwaka 2016/2017, Serikali iliingia mikataba ya ununuzi wa ndege sita. Ndege mbili (2) aina ya Bombardier Dash 8 – Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja ziliwasili nchini Septemba, 2016 na kuanza kazi Oktoba 2016. Ndege moja (1) aina ya Bombardier Dash 8 – Q400 itawasili nchini Julai, 2017; ndege mbili (2) aina ya Bombardier CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 127 kila moja zitawasili nchini Juni, 2018 na ndege moja (1) ya masafa marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 itawasili nchini Julai, 2018.

174.Mheshimiwa Spika, ujio wa ndege hizo mbili aina ya Bombardier Dash 8 – Q400 pamoja na ile iliyokuwepo aina ya Dash 8 - Q300 umeiwezesha ATCL kutoa huduma za uhakika za usafiri wa anga katika maeneo ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, Bukoba, Mbeya, Dodoma, Zanzibar na Moroni (Comoro). Kwa kutumia ndege hizo tatu, ATCL inatarajia kupanua huduma zake katika maeneo ya Mtwara, Mpanda, Songea na Tabora kuanzia mwezi Juni 2017. Safari za nchi jirani za Entebbe (Uganda), Nairobi (Kenya), Bujumbura (Burundi) na Kigali (Rwanda) zitaanza baada ya kupata ndege ya tatu ya aina ya Bombardier Dash 8 – Q400 Julai 2017. Aidha, mara baada ya ndege aina ya Bombardier CS 300 kuwasili nchini, ATCL itaanza safari za kwenda Afrika ya Magharibi, Afrika ya Kati, Afrika ya Kusini, Mashariki ya Kati na India; na baadae kufanya safari za masafa marefu kwenda China, Ulaya, na Marekani baada ya ndege ya Boeing 787 kuwasili.

175.Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017, ATCL ilisafirisha abiria 47,510 ikilinganishwa na abiria 32,434 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2015/2016. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 46. Ukuaji huu ulitokea kati ya Oktoba, 2016 na Machi, 2017 baada ya upatikanaji wa ndege mbili mpya. Katika mwaka 2016/2017, mifumo mipya na ya kisasa ya ukatishaji wa tiketi (reservation system), udhibiti wa mapato (Revenue management system) na uhudumiaji wasafiri uwanjani (Departure Control System) imefungwa. Aidha, ATCL imefungua kituo cha kisasa cha huduma kwa wateja (call centre) ili kuondoa kero zitokanazo na matumizi ya simu za kawaida katika kuhudumia wateja. Lengo ni kuongeza ubora wa huduma zake kwa wateja. Kazi zinazoendelea kutekelezwa ni pamoja kuendelea na hatua za kusafisha mizania ya ATCL; kuimarisha mifumo mbalimbali ya kielectroniki kwa ajili ya uuzwaji wa tiketi za ndege na udhibiti wa mapato ya Kampuni; na kuendeleza raslimali watu ili kuongeza ufanisi.


SEKTA YA UCHUKUZI Makadirio ya Matumizi ya Kawaida na Bajeti ya Miradi ya Maendeleo

335. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Kampuni ya Ndege (ATCL) imetengewa shilingi milioni 500,000 kwa ajili ya kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege 3 ambapo ndege mbili (2) ni za aina ya CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 127 kila moja na ndege kubwa moja (1) ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262. Aidha, fedha hizo pia zitatumika kwa ajili ya gharama za bima, mafunzo (marubani, wahandisi na wahudumu), gharama za kuanzia (start up cost) pamoja na malipo ya awali ya ndege nyingine ya aina ya Boeing 787 (Dreamliner).

336. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma zinazotolewa za Wakala wa 193 Ndege za Serikali. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imetenga Shilingi milioni 10,000 kwa ajili ya kufanyia matengenezo ndege 4 za serikali ili kuhakikisha kuwa huduma ya usafiri wa anga inatolewa kwa Viongozi Wakuu wa Kitaifa ni ya uhakika, salama na inayokidhi viwango.

337. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga imetenga fedha ili itatekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha shughuli za udhibiti wa usafiri wa anga. Miradi hiyo ni pamoja na: i. Kuboresha miundombinu pamoja na huduma za usafiri wa anga nchini; ii. Kuendelea kutoa huduma za uongozaji ndege kwenye eneo la Bahari ya Hindi hadi umbali wa nyuzi 44 mashariki; iii. Kuendelea na juhudi za kuendeleza ujenzi wa chuo kipya huko Fukayose - Bagamoyo ili kuhakikisha chuo kinadahili wanafunzi wengi ambao watahitimu katika nyanja ya usafiri wa anga; iv. Kufunga mtambo wa ILS –Zanzibar; na v. Kununua na kufunga Rada nne (4) za kuongozea ndege za kiraia.


Kuipata hotuba kamili, bofya hapa http://www.mwtc.go.tz/uploads/publications/en1493281737-HOTUBA%20WUUM%202017-2018.pdf


Comments

Most Viewed Posts

Job Opportunities at Air Tanzania (ATCL)

VACANCIES ANNOUNCEMENT Air Tanzania Company Limited (ATCL) is in the process of revamping its operations and has introduced new equipment to its fleet. The Company is therefore inviting applications from qualified personnel to fill various positions. 1.      POSITIONS:  1.1. Dash 8 – Q400 Mechanical and Avionics Certifying Engineers (6 POSTS)     a)    Qualifications·         ·          Must possess a valid Aircraft Maintenance Engineers License (ICAO TYPE II).  ·         ·          Must possess a valid Dash 8 – Q400 Approval/License. ·      Must have successfully completed Dash 8 – Q400 type course from an Approved Training Organisation.        ·       Must have Aircraft Maintenance working experience, as a certifying engineer, of not less than 5 years; 2 of which being on Dash 8 – Q400. Experience must include release to service certification after “A” Check and above.        ·          Computer literacy·         ·          Fluency in English·        

Job Opportunities at Air Tanzania: Pilots-in-Command, Co-Pilots,Aircraft Maintenance Engineers and Cabin Crews.

Air Tanzania Company Limited (ATCL) is in the process of revamping its operations and has introduced new equipment to its fleet. The Company is therefore inviting application from qualified personnel to fill various positions. 1. POSITIONS: 1.1  Pilot-in-Command – Dash 8 (11 Posts) a) Qualifications: Must possess Airline Transport Pilot License (ATPL) and with performance “A”.Must additionally achieve the following:- ·          Minimum of 4000 hours flying experience of which 2000 hours must be command on multi-engine  aircraft; Above 17 ton. ·          Group 1 endorsement on DASH 8 or Equivalent with a minimum of 500 hours command on type; ·          Pass an oral interview and flying acceptance check conducted by the Company; ·          Must pass a Base and Route check with an Instrument Rating within 10 and 70 hours respectively; ·          Track record of good performance as a Commander and no accident record. b) Duties and responsibilities : ·      

Job Vacancy At Precision Air - Cabin Crews (10-Posts)

                                                                                                                  JOB VACANCY Precision Air Services Plc is a fast growing private Tanzanian airline which operates in Partnership with Kenya Airways, with its strategies to expand wings beyond East Africa and Africa. In order to keep our services at a higher level and meet our customers’ maximum satisfaction We wish to invite applications from suitably qualified candidates to fill in this challenging position. POSITION:           CABIN CREWS(10-POSTS) REPORTS TO:     CHIEF CABIN CREW DUTY STATION: DAR ES SALAAM                            ROLE PURPOSE OF THE STATEMENT You will be reporting to Chief Cabin Crew/Assistants Chief Cabin Crew - Precision Air Services PLC. Please take note of your responsibilities. Consistently give quality customer service to passengers in a safe environment for their comfort and satisfaction KEY ACCOUNTABILITIE